MKUTANO WA NNE WA BLW UNATARAJIWA KUANZA RASMI SEPTEMBA 9

Posted on: 07.09.2026
MKUTANO WA NNE WA BLW UNATARAJIWA KUANZA RASMI SEPTEMBA 9, 2026
Mkutano wa nne wa Baraza la Kumi na Moja la Wawakilishi Zanzibar unatarajiwa kuanza siku ya Jumatano tarehe 09 Septemba, 2026 saa 3:00 asubuhi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Kaimu Katibu wa Baraza la Wawakilishi Ndg. Ramadhan Khamis Juma amesema Afisi ya Baraza la Wawakilishi imepokea na kuratibu maswali 302 kwa ajili ya mkutano huo.
Akitaja shughuli nyengine zinazotarajiwa kufanywa katika Mkutano huo Ndg. Ramadhan amesema ni pamoja na Miswada miwili ya Sheria ambayo ilisomwa kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa Tatu na kujadiliwa katika Mkutano huu.
Akiitaja Miswada hiyo amesema Mswada wa kwanza ni Mswada wa Sheria ya kufuta ya Sheria ya kuanzisha Shirika la Magazeti ya Serikali, Nam. 11 ya 2008 na kutunga upya Sheria ya Shirika la Magazeti Zanzibar kwa Madhumuni ya Kuendesha Biashara ya Magazeti na kuweka Mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Mswada wa Pili ni Mswada wa Sheria ya kufuta sheria ya uvuvi, Nam. 7 ya 2010 na kutunga Sheria ya Mamlaka ya Maendeleo ya Uvuvi na Uhifadhi wa Bahari kwa ajili ya kusimamia, Kuendeleza uvuvi na Kuhifadhi Maliasili za Bahari na kuweka Mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Aidha, akifafanua Shughuli nyengine itakayojadiliwa katika Mkutano huo Ndg. Ramadhan amesema ni pamoja na Hoja ya Marekebisho ya Kanuni za Kudumu za Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Toleo la 2024.
Shughuli nyengine inayotarajiwa kujadiliwa katika Mkutano huo ni Taarifa ya Serikali kuhusiana na Hali ya Dawa za kulevya Zanzibar ya Mwaka 2025.